Mwanafamilia ya Baba wa Taifa, Vincent Nyerere (35), pichani, wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anakusudia kuwania ubunge katika Jimbo la Musoma Mjini linaloshikiliwa na Vedatus Manyinyi wa CCM. Akizungumza na gazeti Nipashe mjini Musoma mwishoni mwa wiki iliyopita, Vincent, alisema ameamua kuwania kiti hicho ili aweze kuwasilisha mawazo na kero za wananchi wa jimbo hilo bungeni. Alieleza kuwa matatizo yanayowakabili wakazi wa jimbo hilo bado hayajatatuliwa kikamilifu likiwemo tatizo la ukosefu wa dawa hospitalini, walimu na huduma ya maji safi. “Kwa bahati nzuri wakazi wa Musoma Mjini tumezungukwa na chanzo kikubwa cha maji yaani Ziwa Victoria lakini ni asilimia ndogo sana ya wananchi wa hapa wanaopata huduma ya majisafi…tena hali ni mbaya zaidi katika Kata ya Nyakato,” alisema. Alisema watu wengi wa manispaa hiyo wanafuata maji ziwani badala ya kuunganishiwa mabomba ili huduma hiyo ipatikane majumbani. Aidha, Vincent alisema kiwango cha elimu mkoani Mara hasa katika Manispaa ya Musoma Mjini, kimeporomoka kutokana na walimu wengi kukimbilia kwenye shule za binafsi kutokana na maslahi duni pamoja na mazingira magumu ya kazi ikiwemo nyumba za kuishi. Alifafanua kuwa kama akipata nafasi ya kuongoza jimbo hilo, atakuwa mwakilishi muadilifu wa wananchi wa Musoma Mjini huku akitaja vipaumbele vyake kuwa ni elimu na afya. Vincent Nyerere ni mtoto wa mdogo wake hayati Mwalimu Nyerere, marehemu Josephat Kiboko Nyerere ambaye alikuwa kitinda mimba katika familia ya Baba wa Taifa.
Habari chanzo: NIPASHE
No comments:
Post a Comment