Hatimaye Bank ya CRDB imepunguza kero ya wanafunzi wa Mkoa wa Dar es salaam kwa kutoa msaada wa mabasi makubwa 5 yenye thamani ya mil 100 kila moja. Uzinduzi wa mabasi hayo umefanywa jana Dar es Salaam na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete kwa Shirika la Usafiri la Dar es Salaam (Uda) kuhadharishwa mradi usifie mikononi mwake. Waziri Mkuu alitangaza kwamba Serikali iko tayari kuwaondolea ushuru watu binafsi, kampuni na mashirika watakaoguswa na kununua mabasi kwa ajili ya mradi huo uliokabidhiwa Uda kwa mkataba na utaratibu maalumu wa uendeshaji. “Hatutakubali kuona mradi uliozinduliwa leo ukifa au ukapotea kimaajabu tu,” alisema Pinda. Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uda, Martin Milanzi, magari hayo yatatoa huduma kwa njia za Kariakoo-Tegeta, Chanika-Kariakoo na Kariakoo-Mbezi Shamba kwa nauli ya Sh 100 kwa mwanafunzi. Takwimu zilizowahi kutolewa zinaonesha Dar es Salaam yenye wanafunzi zaidi ya 500 inahitaji zaidi ya mabasi 10,000 ya kawaida, kubeba idadi hiyo ya wanafunzi kila siku asubuhi wanapokwenda shuleni na jioni wanaporudi. Mh Pinda alisema “Tujitahidi kuonesha watoto kuwa tunabuni mambo yanayowezekana. Kampuni mbalimbali zione jambo hili ni letu sote. Basi moja ni Sh milioni 100 na ushuru, bila ushuru ni Sh milioni 75. Hili la kuondoa ushuru mabasi yapatikane linawezekana,” alisema Pinda na kumwelekeza Mkuu wa Mkoa, William Lukuvi, wakae kuangalia namna ya kutoa msukumo kwa wengine kuchangia.
No comments:
Post a Comment